Matokeo Mabaya Kidato cha Sita – Mtazamo Wangu

A K Simai

Yalipotoka Matokeo ya kidato cha Nne ambayo yalikuwa mabaya kufikia baadhi ya Skuli za Zanzibar kufutiwa Mitihani pamoja na kufungiwa watahiniwa wote waliothibitika kwamba wamekopia kwa muda wa miaka mitatu kutofanya mitihani (muda huu umepunguzwa sasa na kuwa mwaka mmoja).

Tulisikia jinsi Jumuiya za wanaharakati pamoja na wazee wengi walioonesha hisia zao kustushwa na kusononeshwa na matokeo yale hasa katika suala la kukopia.


Msisimko na mshtusho uliweza kuliweka suala la mitihani kwenye masikio ya wananchi kwa muda wakifuatilia kujua kinachojiri na kuendelea mpaka kutishia kuwafikisha mahakamani vyombo husika endapo haki haitotendeka.

Waliofeli walikuwa ndugu zetu, wanetu, marafiki zetu na tegemeo la nchi kwa siku zijazo.Kwani humo ndimo watakapotoka Viongozi, Wataalamu, Madaktari, wauguzi na kadhalika.


Yalipotoka matokeo ya kidato cha sita ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa mabaya zaidi na yaliyo na athari zaidi kwa jamii hatukusikia kauli yoyote ya nguvu kutoka kwa wahusika, Wizara, au hata wanaharakati na baya zaidi Zanzibar iliongoza katika Skuli zilizofanya vibaya kiujumla.

Kilichonishtua zaidi ni kwamba wanafunzi wote waliobahatika kufanya mtihani wa kidato cha sita ni wale wale waliopasi kidato cha nne vizuri na kupata fursa ya kuendelea na masomo. Je kufeli huku kwa mamia hakuashirii kitu kwamba ufaulu wao wa kidato cha nne labda ulikuwa na walakini? Ni dhana tu inayoweza kuaminishwa na matokeo ya kidato cha sita kwamba labda ina ukweli fulani ndani yake.

Nini maana yake

Katika kufeli Mtihani kuna kitu au sehemu lazima itakuwa tumekosea kama wanafunzi, Wazazi, Walimu, Wizara na hata Necta.

Wanafunzi

Wanafunzi ima hawakuandaliwa au kujiandaa vyema na mitihani hii. Ingawa jitihada kubwa hufanyika ya kusoma pamoja na tuition lakini inawezekana hazilengi katika kufikia lengo la kumwezesha mwanfunzi kupasi mtihani.

Tatizo aidha ni mwanafunzi, au Mwalimu au nyenzo zinazotumika au mfumo unaotumika.

Wazazi

Wazazi wanaweza kuhusika kwa njia moja au nyengine kama kutofuatilia kwa ukaribu maendeleo ya watoto ili kuweza kupata picha halisi ingawa si rahisi kutokana na hali halisi lakini kumuona mtoto anatoka tu na kwenda skuli na kisha tuisheni bila ya kuwa na uelewa kitu gani anakifanya na changamoto gani anakabiliana nazo kunaweza kuchangia matokeo mabaya ya mtoto.  Kwa mfano Je mzazi aliwahi hata mara moja kwenda skuli kukutana na Walimu wa mwanafunzi kujua maendeleo yake au hata matatizo?

Tatizo Upeo, muda na uelewa wa wazazi katika kufuatlia maendeleo ya watoto.

Walimu

Tukija kwa Walimu ima hawana uwezo au upeo wa kukabiliana na changamoto hii au mazingira yanayotumika kufundishia hayakidhi viwango au  kutokuwa na nyenzo muwafaka za kufundishia.
Tatizo aidha ni Mwalimu, Mfumo au Wizara husika.

Wizara

Tukija kwa Wizara inayosimamia elimu inawezekana ilikurupuka au ilishtushwa na wimbi la ongezeko la wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na hivyo kujikuta kuingia katika hali iliyolazimku kufungua sekondari nyingi za kidato cha tano na cha sita bila ya kuwa na mipango madhubuti ya kupata kwanza Walimu wenye sifa na pia mazingira muwafaka.

Pia kuanzishwa kwa vyuo vikuu ambapo mahitajio ya wanafunzi kuongezeka  inawezekana Wizara ilijikuta katika wakati mgumu wa kukubaliana na changamoto hizi bila ya kuwajengea mazingira sahihi Walimu pamoja na wanafunzi. Hatimae tunavuna kile tulichokipanda

Tatizo Aidha ni  Wataalmu na Watendaji wa Wizara nao hawakuona mbali na kuwa na upeo, Kutokuwa na fedha za kusimamia zoezi la kuboresha mazingira ya masomo katika Maskuli ya aina hii. Vitendea kazi kutokuwepo vya kutosha katika maskuli na kadhalika.

Necta

Mwisho ni Necta Je katika utungaji na usahihishaji wa mitihani kuna mfumo ambao uko fair na transparent kwa wote na vipi mitihani huweza kuvuja kila mwaka mpaka wengine kuweza kuipata mapema?
Tatizo ni Necta yenyewe, mfumo wake au kuna na jengine?

Ukiangalia kwa ujumla utakuta kufeli kwa watoto wetu si suala la wanafunzi pekee bali ni suala ambalo linakwenda mbali sana na kugusa sehemu tofauti kwa mtazamo wangu finyu.

Hii kwa maoni yangu ni aibu ambayo kama ni wizara husika basi ingeliona haja ya kufanya uchunguzi – inquiry kujaribu kuona mapungufu yaliyojitokeza na vipi yataweza kurekebishika na matokeo ya uchunguzi huu kuwekwa hadharani kwa faida ya wote.

Nchi ya Finland katika nchi za Ulaya ni moja katika nchi zizlizopiga hatua kubwa katika masuala ya elimu. Imeweza kuzipita nchi nyingi kubwa katika maendeleo ya kielimu kwa sababu waliamua kuwekeza katika Elimu. Kazi ya ualimu nchini Finland ni kazi ambayo kila atakaemaliza masomo hutaka kujiunga nayo kwa kuwa ina mshahara mzuri pamoja maslahi kadha wa kadha.

Sikusudii kufanyika marekebisho ya sekta ya Walimu katika Mshahara ila ni kutoa mfano vipi wenzetu wanavyotaka kuleta mapinduzi ya kifikra katika nchi zao wanavyojipanga  na kulenga eneo muhimu la elimu.

Kama hatua  madhubuti hazijachukuliwa sasa kuna hatari ya kukiandaa kizazi kijacho tutakachokibebesha majukumu kikiwa hakina upeo wala uwezo wa kukabiliana na changamoto za hali halisi inayowakabili ya kuwaletea maendeleo wananchi na Taifa  la Zanzibar.

13 comments:

  1. Nadhani maoni yako ni sawa na yote yanajikita katika tatizo moja kubwa: WALIMU. Zanzibar hakuna walimu wa kutosha na wenye viwango katika elimu ya sekondari na juu. Lakini tatizo la ubora haliko kwa elimu tu. Watu wanazungumzia wanafunzi kufeli na kuhusisha walimu kwasababu kuna kigezo cha mtihani kupima ubora wa wanafunzi. Kwahiyo kama output haikuwa nzuri tunajua kuwa kuna tatizo. Lakini kwa bahati mbaya hakuna vigezo vya wazi vya kupima ubora wa huduma au output za idara au maeneo mengine. Kwa mfani vipi utaweza kupima ubora wa Idara ya Maji, Hospitali, wizara ya kilimo na kadhalika?
    Wakati umefika kwa Zanzibar kwa wizara zote kuajiri watu kulingana na ubora wao na sio vyeti vyao.Hii ni mada pana mno lakini nahisi mchangi huu unatosha.
    Mwisho nataka kuuliza jee ni vipi tutaweza kupima ubora wa wahitimu wa vyuo vikuu vyetu? Jee Division waliopata au kwa uwezo wao wa kazi?

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli tasnia ya elimu Z'bar ina matatizo mengi, kiasi kwamba ukianza kuelezea huwezi kumaliza.

    Lakini mimi kwa upande wangu nasikitishwa sana na upungufu wa walimu wenye viwango stahiki!

    ReplyDelete
  3. Nakubaliana na michango ya waliotangulia. Lakini pamoja na sababu mlizozitaja,msisahau kwamba,Z'bar bado hatujawa serious kwenye masuala ya elimu n.k. Kwa mfano,tutategemea vipi ufaulu mzuri wa wanafunzi wetu,ilhali walimu wanaowafundisha walikuwa failures?! Ukifanya utafiti,utagundua kuwa,walimu wengi tulionao maskulini,ni wale ambao walifeli huko nyuma na wakaamua kwenda kusomea ualimu kwavile hawakuwa na option nyengine. Hali hii pia tunaiona hata madaktari wetu 'watarajiwa' walioko Chuo cha afya (Mbweni). Wengi wao wanajiunga na chuo kwa 'zengwe' na kujuana badala ya sifa stahiki. Jee,kwa mazingira kama haya,kweli tutegemee madaktari wazuri wa kututibu? Jawabu ni kwamba hapana. Imefika wakati sasa,serikali ibadilike. Badala ya kuangalia'quantity' saivi izingatie 'quality'. Isijikite kuanzisha maskuli mengi yasiyokuwa na tija na badala yake kuwe na skuli chache ambazo zitazalisha 'products' zenye ubora. Wenzetu katika nchi zilizoendelea,huajiri wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao na wale wenye 'potentials' kuwa walimu,madaktari,mainjinia,wanasheria n.k. Na pia wanawalipa vizuri tu. Hii ni kwasababu,hizi ni miongoni mwa fani zinazohitaji watu walio 'smart' na sio 'wababaishaji'
    Naomba kuwasilisha.

    ReplyDelete
  4. Ahsante mtoa mada angalau kwa kuliona jambo hili na ukaweza kulijadili kwa kiasi fulani, binafsi naunga mkono katika maeneo mengi ambayo umeyazungumza, lakini zaidi na zaidi nahisi kwamba tatizo liko kwa Serikali pamoja na Wizara ya Elimu, kwani wanaonekana kuendelea kutokujali licha ya matokeo mabaya ya mitihani katika miaka iliopita.Wanaonekana kufumbia macho matokeo mabovu yanayozikumba shule zetu za Zanzibar. Kimsingi Serikali kupitia Wizara husika walipaswa kusimamia kikamilifu suala la utoaji wa elimu visiwani humo, ikiwa ni pamoja na kuandaa na kuwawezesha walimu kukabiliana na changamoto za taaluma, aidha kuandaa vifaa vya maabara, kuhakikisha upatikanaji wa vitabu vya ziada na kiada kwa wanafunzi na waalimu nk. Aidha jamii kwa ujumla inapaswa kuamka na kuguswa na hali mbaya ya matokeo ya ndugu zetu, tunapaswa kuisindikiza Serikali ili iweze kutilia maanani suala zima la elimu kwani bila ya elimu bora hakuna maendeleo.

    ReplyDelete
  5. Jamani sio kila kitu ttzo ni serikali tu, kwani hapa znz si kuna shule za binafsi? mbona nao taabani?au nazo pia ttzo ni serikali? ttzo lenu kila kitu mnakitia siasa wazanzibar, acheni siasa kuna mambo mengine yanataka skills.

    ReplyDelete
  6. Nianze na mtowa maoni wa mwisho serikali lazima ihusishwe na matokeo mabaya ya ufaulu wa wanafunzi. Hizo skuli bibafsi ni output hiyo hiyo ya wizara ya elimu au mfumo mbaya wa elimu Zanzibar. Wizara inaendeshwa kwa uzoefu sio utaalamu, tatizo watu wengi hawaijui wizara ya elimu. Watendaji wake wameoza na haya ndio matunda Jiulize ni nani mkuu wa ukaguzi, wa mitihani, mitaala na wngineo katika wizara. Jiulize ni wangapi wenye specilization kwenye maeneo wanayo yaongoza. Mabadiliko hayatapatikana kwa uongozi wa kubahatisha. Wizara daima inategemea misaada hata kwa mabo madogo madogo. Hakuna mafunzo kazini angalau kupiga msasa walimu ukiyaona hayo basi ni mradi tena wala si miongoni mwa mambo endelefu yenye kuwajengea uwezo walimu.

    ReplyDelete
  7. Nawashuru watoa maoni wote kwa michango yenu mizuri na ule wa kipekee wa mchangiaji wa tatu juu.

    Hata hivyo mimi ningependa tu kutilia mkazo ktk mambo mawili ambayo ni;
    Mwamko mdogo wa jamii ktk suala la elimu na ubovu wa waalimu.

    Inasikitisha kuona kwamba hadi leo hii, jamii yetu bado haijatoa umuhimu unaostahiki ktk suala la elimu.
    Hapa kwetu ni kawaida kuona mzazi ambae hajui hata mtoto wake yuko darasa la ngapi, seuze kujua maendeleo yake!
    Wengine wanafikia hadi kutoroka skuli bila waazazi wao kujali

    Wenzetu hapo Bara tu, wanachukulia elimu ya watoto wao kua ni 'jihadi' utakuta mzazi anauza vitumbua lkn. anasema 'nashukulu, mtoto waangu anaenda shule' sisi tulioambiwa 'ikra!' tunazembea!

    Ama kwa upande wa waalimu ndio usiseme, walimu ni wabovu kupita kiasi, hivi, inaakuwaje mwalimu wa sekondari hasa ktk karne ya leo ashindwe hata kwenda kwenye GOOGLE kutafuta materials ya kufundishia kama kweli anaipenda kazi yake na huduma za internet ni 500 tu kwa nusu saa! na kwenye neti kila kitu kinapatikana!

    Nnapozungumzia ubovu wa waalimu nna uhakika na hilo: Waalimu ni ndugu zetu, wengine wake zetu, marafiki zetu na hata classmates wetu!
    Mfano mimi mwenyewe ni mwalimu kitaaluma na nimeitumikia wizara ile kwa tariban miaka 10! mtu hana cha kunieleza.

    Ndugu zetu MWAMSHO watusaidie ktk hili pia kama kweli wanavitakia visiwa hivi lau kama wana ajenda nyingine sawa!!

    ReplyDelete
  8. Ukweli wa kutatua tatizo la elimu Zanzibar lipo mikononi mwa wazazi na wanafunzi wenyewe. Pamoja na serikali kuweka miundombinu muafaka ya kupatikana kwa elimu bado jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri lipo mikononi mwa wazazi na wanafunzi wenyewe. Mwamko wa kupenda kusoma na kujifunza Zanzibar uko chini mno ukilinganisha na bara. Kuna mifano hai kabisa kwa baadhi ya wazazi walioamua kwa makusudi kabisa kuwapeleka vijana wao bara kupata elimu wamekuwa na mitazamo na mafanikio makubwa kulinganisha na wale waliopo hapa. Ninachotaka kueleza hapa ni kuwa wazazi wenye uchungu na uelewa wa elimu wanalazimika kuhangaika huku na kule kutafuta mafanikio ya watoto wao.
    Inasikitisha sana unapokuwa maeneo ya mjini kama Forodhani nyakati za jioni na hata usiku ndani ya week days unakuta vijana wa shule wakipoteza mida mingi kwa mambo ambayo si ya lazima ilhali katika mida kama hiyo watoto waliopo bara hasa boarding schools wakiwa wanajisomea. Aidha, ukikatiza mitaa ya michenzani roundabout na sehemu nyinginezo, utashangaa kuona watu wengi hasa wazazi wa kiume wakitumia muda wao mwingi kwa kukaa maskani kwa mazungumzo badala ya kutumia muda huo vizuri kwa kuwa majumbani mwao kuhimiza au kusimamia malezi ya watoto hasa kuhakikisha wanajisomea. Inapofika wakati wa kutoka majibu ya mitihani, vijiwe hivihivi ndiyo vinavyoongoza katika kulaumu asasi zingine kwa matokeo mabaya bila ya kujali nini ilikuwa mchango wao katika kuhakikisha kadhia kama hiyo haitokei. Tufike wakati sasa tuambiane ukweli na kuondoa dhana ya kwamba wazanzibari tunaonewa ilhali hatutimizi wajibu wetu ipasavyo. Kama alivyogusia mchangiaji mmoja hapo juu kuwa kuna wazazi hawajui hata watoto wao wanasoma darasa la ngapi, mimi ninaongezea kuna wazazi hawajawahi hata kujua mtoto wake anasoma nini shule, kuna wazazi ambao hawajahi kuonana na hata mwalimu wa mtoto wake tangu ameanza shule.
    Endapo wazazi watafuatilia maslahi ya watoto kielimu basi mamlaka zingine zote zilizobaki zitarekebishika na kukaa kwenye mstari. Endapo kama shule ina waalimu waso na sifa bafa basi wazazi watakuwa na ukweli juu ya wahusika na hatua za kurekebisha zitachukuliwa. Endapo mitaala haifai basi wazazi wataona kutokana na mapitio yao ya kila mara. Tusijaribu kufanya majumuisho na kuhitimisha kuwa matatizo ni waalimu, au mifumo wakati kiungo muhimu kabisa katika elimu 'wazazi' hakifanyika kazi yake ipasavyo.
    Katika utafiti wangu inaonesha kuwa ushirikiano katika ya wazazi-walimu ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya elimu.

    ReplyDelete
  9. Inaonesha wenye akili Zanzibar wapo lakini tu...
    Hii michango ni mizuri kuliko hata ya baadhi ya wawakilishi.

    ReplyDelete
  10. Baada ya kupitia michango na maoni ya waliobahatika kusoma makala hii na kuona haja ya kuchangia nimeweza kufarijika na jinsi wachangiaji walivyoonesha kuguswa na jambo hili na pia kwenda deep zaidi ya mtoa mada katika kuchambua na kudodosa matatizo yanayoikabili sekta ya Elimu Zanzibar.

    Kwa vile niliichokoza mada hii na kuweza kupata maarifa zaidi nimeona iko haja ya kuitanua na kujumuisha nukta zilizoorodheshwa ili ikae katika mfumo wa kitaalamu na kitaaluma na ninaamini inaweza ikawa moja katika papers ambazo zitaweza kufanyiwa presentation kwenye Semina, Warsha na hata kwa Wazazi ili waweze kuipata picha halisi ya kiini cha matatizo ya Elimu na huku tukiendelea kutafuta long and short term solutions InshaAllah.

    Tunawashukuru wote

    A K Simai

    ReplyDelete
  11. Ikiwa ni ktk muendelezo wa kuchangia maoni juu ya mada iliyotolewa na ndugu yetu kuhusu elimu Z'bar, kuna jambo ambalo nimeliona na limekua likiniumiza sana kichwa.

    Jambo hili si jingine bali ni ukosefu wa kujiamini (confidence) kwa wanafunzi wengi wa Zanzibar. Kilema hiki hakiishii tu kwa
    Wanafunzi bali pia Waalimu, Wanasiasa na hata viongozi wa serikali.

    Baada ya kuona 'maafa' ya kukosa 'confidence' kwa viongozi wetu mbali mbali na wasiasa hasa wale wanaohudumu ktk taasisi za muungo likiwemo bunge, nilijaribu kumuuliza rafki yangu mmoja ambae ni mtaalamu wa mambo ya mitaala.

    Kijana yule wa kizanzibari alikiri kuwepo kwa tatizo hili na kuniambia kwamba linatokana na mfumo wetu mbaya wa elimu lkn. wengi wetu hapa Z'bar hatukubali hili ingawa tunawaona wenzetu upande wa pili wa jamuhuri(bara) wakifanya vizuri ktk hilo!

    Alisema ktk elimu kuna CORE AND EXTRA CURRICULLUM ACTIVITIES ambavyo vyote, walimu wanapaswa kuvizingatia ktk ufundishaji kama kweli tunataka watoto wetu waelimike.

    Alidai walimu wengi hapa hawajui kua, vitu kama DEBEAT maskulini vinasaidia sana wanafunzi kujiamini, kupata uwezo wa kuhoji mambo na kuzungumza mbele za watu, wao wanadhani mambo hayo watu huzaliwa nayo tuu!
    Si, ajabu hapa kukuta mw'funzi wa chuo ambaye tokea primari hajawahi kusimama mbele ya darasa kuuliza au kueleza kitu labda alazimishwe na mwalimu, matokeo yake akisimama mbele za watu au kuhojiwa na chombo cha khabari anashindwa.

    Sisi tunabaki,..ah yule ana nadigrii/ masters.. hivoo! kumbe kuzungumza kitu mbele za watu hawezi, wengine hata kiswahili wanakosea, kwa kukosa kujiamini!

    Wenzetu wamefikia hata kua na wasiwasi kutuchagua ktk baadhi ya nafasi zikiwemo zile za kimataifa. hebu jamani tujitathmini kwa maslahi ya watoto wetu na Taifa letu.

    Mungu ibariki Zanzibar!

    ReplyDelete
  12. Ningependa kurudi hapa na kukupongeza Ndugu yangu A. K. Simai kwa kuchokoza mada hii na kutuleta wachangiaji hapa kuweza kujadili mambo yanahusuhu elimu ndani ya Zanzibar. Nimetoa maoni yangu hapo juu na nimefarijika zaidi na maoni ya wachangiaji wengine japo baadhi tumetofautiana katika hoja. Lakini wote tumekuwa na lengo moja la kutafuta suluhu ya kadhia inayokabili taifa. suala la matokeo mabaya ya watoto si athari yao au wazazi wao tu bali hata taifa kwa ujumla. Katika maoni yangu nilisisitiza uwajibikaji wa wazazi kama kiungo muhimu natumaini kuwa wengi wetu tutaona umuhimu wa wazazi katika kusimamia nafasi yao kikamilifu.
    Hakuna lisilowezekana kama kila mtu atatimiza wajibu wake.
    iskitogo@gmail.com

    ReplyDelete
  13. Tuition kwa kiasi kikubwa zinatuponza wanafunzi wa Zanzibar, nimesoma SOS na kumaliza 2010 kidato cha sita,nashukuru Mungu nipo St. Augustine Uni nasoma Degree ya Ualimu.kilichonifanya nisomee ualimu ni mambo ambayo hapo juu tumezungumzia, walimu wetu wengi ni Diploma holders na Certificate hasa wa O'level na Advance level kwa shule nyengine.Mwalimu anafundisha kidogo tu na kusahau Curriculum(mhuktasari) unataka nn, walimu wetu wanashindwa hata kumaliza silabus, na NECTA wanatoa mwanzao hadi mwisho wa SILABUS, lazima wanafunzi wafeli na ndipo tunapokimbilia tuisheni.ili kumaliza SILABUS nzima, walimu wanafundisha kwa uzoefu wao wa miaka 1967 waliosoma wao, wakati mambo mengi yamebadilika..Kama motisha naomba tuwepamoja hata kuwahimiza vijana tujaribu kusoma na kuona namna gani tutasaidia jamii yetu, sio wote kusoma IT, Ugavi, Business nani atakuwa mwalimu bora kwa wadogo zetu na watoto wetu hapo baadae?? tujenge sasa ili hapo baadae tuwe pazuri...

    Remy Mkwaya
    St.Augustine University of Tanzania
    MWanza
    remytothenet@gmail.com

    ReplyDelete

ZanziNews Templateism Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.