Habari za Punde

7OOO WAKABILIWA NA UPUNGUFU WA CHAKULA MICHEWENI

Balozi Seif azitaka Kilimo, Fedha kutafuta ufumbuzi haraka

Na Mwantanga Ame, Pemba

TATIZO la uhaba wa chakula limejitokeza tena katika wilaya ya Michweni na kusababisha wananchi zaidi ya 7,000 wa maeneo hayo kukumbwa na upungufu mkubwa wa chakula cha mazao.

Hali hiyo imejitokeza kwa muda wa miezi mitano sasa baada ya eneo kubwa la mashamba ya wakulima kutokuwa na uzalishaji wa chakula cha aina yoyote.

Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi ambae alikuwa ziarani kisiwani Pemba, ameshuhudia kuwepo hali hiyo na kuwapa pole wananchi wa wilaya hiyo na kuahidi serikali kulifanyia kazi tatizo hilo.

Sehemu kubwa ya eneo hilo imeonekana ikiwa haina ana yoyote ya uzalishaji wa chakula huku baahi ya migomba ilikiwa imekufa.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, akitoa maelezo ya hali hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais, alisema hali hiyo imekuwa ikijirejea mara kwa mara na tayari serikali ya wilaya imeshawasilisha mapendekezo ya kuchukuliwa kwa hali ya dharura kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa tatizo hilo ni wengi wa wakulima wa maeneo hayo hutegemea kilimo cha mvua.

Aidha alisema tatizo kubwa zaidi ni baadhi ya wananchi kuwa wakaidi wa kufuata maelekezo kutoka kwa wataalamu katika shughuli za kilimo.

Akifafanua kauli hiyo alisema baadhi ya wakulima walishauriwa kupanda vyakula vinavyostahmili ukame kama mtama na uwele, lakini walikataa na kuendelea kupanda mihogo.

Hali hiyo alisema ndio chanzo kikubwa cha kutokea upungufu wa chakula kwa vile tayari ardhi ya maeneo hayo haikubaliani na vipando vya aina hiyo kutokana na kuwa kame.

Baya zaidi alisema sehemu wananchi wanaoshughulika na kazi hizo ni wanawake huku wanaume wengi huenda kuvua katika utaratibu wa kambi za dago ambapo huchukua zaidi ya miezi mitatu kurudi nyumbani.

Aidha, Dadi alisema matayarisho waliyoandaa ni kuwaweka wakulima wa wilaya hiyo katika vikundi sita kutoka katika shehia sita, ambazo zitahitaji kupatiwa fedha zisizopungua shilingi 500,000 hadi 600,000 ili vianzishe shughuli za kilimo cha umwagiliaji na kazi za ufugaji.

Alisema mapendekezo hayo hivi sasa yanasubiri kupata fedha kutoka serikalini huku serikali ya mkoa ikiwa inaendelea kuchukua hatua za dharura juu ya suala hilo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema wengi wa wananchi hivi sasa wamekuwa ni wenye hali ngumu kukabiliana na tatizo hilo kutokana na kutegemea kupata chakula cha kununua huku kikiwa kimepanda bei ambapo mchele wa mapembe unauzwa shilingi 1,00 kwa kilo na unga wa ngano unauzwa shilingi 1000.

Mmoja wananchi ambaye alizungumza na Zanzibar Leo, Hamad Juma, alisema hali hiyo imewaathiri kwa kiasi kikubwa na wamekuwa wakitegemea kupata chakula zaidi cha kununua madukani na hakuna anaekula chakula cha mizizi.

Kwa upande wa Balozi Seif, alisema hali iliyojionesha katika eneo hilo ni ya kusikitisha na kumtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Khalid Salum Mohammed, kulifanyia kazi kwa haraka suala hilo kwa kushirikian na Wizara ya Fedha.

Alisema jambo linalosikitisha ni kuona wananchi wanakosa fedha za kununulia chakula huku wakikabiliwa na njaa jambo ambalo litaweza kuleta maafa.

"Hali ni mbaya mazao hayaji, vyakula bei mbaya lazima watafutiwe njia bora,” alisema Balozi Iddi.

Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais, ameridhika na hatua ya ujenzi wa skuli ya sekondari ya wilaya unaofanyika Tumbe, ambapo aliwataka watekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanaukamilisha kwa wakati uliopangwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.